U.S. Markets closed

MUHTASARI: Mechi za La Liga, Messi aweka rekodi mpya

Messi aweka rekodi mpya Barca ikishinda 4-0 dhidi ya Deportivo La Coruna

Ilikuwa ni Jumamosi nzuri kwa upande wa Barcelona wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Camp Nou.

Miamba hiyo ya Catalan ilifanikiwa kunyakua pointi tatu kwenye mchezo wa LaLiga baada ya kuifunga Deportivo La Coruna kwa bao 4-0.

Rafinha alifunga magoli mawili kabla ya Luis Suarez kufunga bao la tatu katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Leo Messi alifunga bao la nne na kukamilisha ushindi kwa upande wa Barcelona.

Bao la Messi dhidi ya Deportivo limempa rekodi mpya ndani ya soka la Hispania.

Leo Messi sasa amekuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi kwenye mechi za ligi katika uwanja wa nyumbani akiivunja rekodi ya mkongwe wa Athletic Bilbao Telmo Zarra.

Zarra alikuwa amefunga magoli 179, wakati Messi sasa amefikisha magoli 180.

Star wa Real Madrid Cristiano Ronaldo anashika nafasi ya nne akiwa na magoli 150 kwenye La Liga mechi ambazo timu yake imecheza uwanja wa nyumbani.

Isco atupia mbili Real Madrid ikiibuka na ushindi wa 6-1 dhidi ya Real Betis

Real Madrid nayo iliibuka na ushindi wa 6-1 dhidi ya Real Betis Isco akiwa kinara wa mabao wa mechi kwa kutupia mbili, na Ronaldo kama kawaida yake.

Kiungo wa Real Madrid Isco ameelezea furaha yake baada ya kufunga mara mbili Los Blancos wakiibuka na ushindi huo mnono Jumamosi usiku.

Nyota huyo wa Kihispania amekuwa akihaha kupata namba kwenye kikosi cha Zinedine Zidane katika mechi za awali, lakini alifanya maajabu katika mechi dhidi ya Betis La Liga.

Ilidaiwa kuwa Isco alikuwa na mahusiano mabaya na kocha wake Zinedine Zidane, lakini nyota huyo, 24, ameeleza kuwa kocha wake anampa uwezo wa kujiamini zaidi.

Isco alihusishwa sana na tetesi za kutaka kutimkia Tottenham Hotspur dirisha la uhamisho wa majira ya joto.

Carrasco atisha kwa hat-triki Atletico Madrid ikiipiga wiki Granada

Bosi wa Atletico Madrid Diego Simeone amesema Yannick Ferreira Carrasco ni mchezaji ambaye kila anachokifanya hufanya katika ubora wa hali ya juu baada ya kupiga hat-triki timu yake ikishinda 7-1 dhidi ya Granada katika La Liga.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amekuwa akitajwa kutakiwa na Barcelona na Chelsea wiki za hivi karibuni baada ya kudhihirika wazi kuwa nyota huyo aliyetua Hispania akitokea Monaco mkataba wake una kipengele kinachomruhusu kununuliwa kwa takribani paundi milioni 34.

Carrasco pamoja na tetesi zote hizo amesema anafurahia kuwa Atletico. Meneja wake amefurahishwa na kiwango chake kikubwa alichoonyesha Jumamosi.